NEEMA YA MUNGU IOKOAYO

 

Friday, January 4, 2013




(Tito 2:11) Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote IMEFUNULIWA

Siku zote katika maisha unaposikia kitu kimefunuliwa, basi ujue ya kuwa kitu hicho kina uwezo wa kufunikwa, neema ninayoizungumzia ni neema kwa ajili ya wanadamu wote haijalishi dini, umri, rangi, jinsia, tajiri au masikini ili mradi unayo pumzi ya uhai. Neema hii itakuja kufunikwa siku moja, mimi na wewe hatujui, ila siri hii ipo kwa Mungu tu, Mungu ameificha kwa makusudi yake.
(Mithali 25:2) Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo; Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo.

Uhai tulio nao ni neema ya Mungu, kwetu sisi wanadamu yu mkini kuna kitu sijakikamilisha Mungu anataka nikikamilishe kabla muda wangu wa kuishi hapa duniani haujafika mwisho.
(Mathayo 24:36) Walakini habari ya saa ile na siku ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni , wala mwana , ila Baba peke yake.

Unaposikia fulani amefariki,basi nawe ujiandae ili itakapofika siku yako, uwe na ujasiri mbele za Mungu, maana ndiko tunakokwenda binadamu wote, kutoa hesabu ya matendo yetu kwa yote tuliyofanya hapa duniani. Katika vizazi vilivyopita biblia inatuonyesha, baadhi ya watu au viumbe walioichezea neema wakaijutia, bila ya kupata neema ya kutubu na kutengeneza na kujirekebisha, pamoja na kuitamani tena kwa machozi, neema ijirudie haikuwezekana.

1.TAJIRI: (Luka 16: 19-31)  Akasema palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula siku bzote kwa anasa.Na masikini mmoja jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani ...

2.LUCIFER/SHETANI:  (Ezekiel 28: 14-15)  Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe yenye moto.
Kabla hajafanya dhambi aliyokusudia moyoni mwake, Mungu aliigundua nia yake ovu na kutoa adhabu, hakukuwa na nafasi ya kutubu, kutengeneza, neema kwake lucifer/ shetani ikaishia hapo. Kabla ya kuasi Lucifer/Shetani alikuwa karibu na Mungu mno kuliko hta sisi binadamu, tena alimjua na anamjua Mungu mno kuliko hata sisi binadamu (Yakobo 2:19) Wewe waamini kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka.
3. KIZAZI CHA NUHU: Watu wa kizazi cha Nuhu, waliichezea neema, pamoja na kuhubiriwa mara nyingi sehemu mbali mbali, hawakubadilika, neema ilipofunikwa pale gharika ilipoanza ilishindikana kujiokoa kabisa pamoja na ujuzi wa kuogelea karibu na mlango wa safina haikusaidia. Maana aliyefunga mlango (neema) alikuwa ni Mungu mwenyewe. (Mwanzo 7:16) Na walioingia, waliingia mume na mke, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyomwamuru Mungu; Bwana akamfungia.

Hata siku ya mwisho atakaporudi Yesu, atakaye funga neema atakuwa ni Mungu mwenyewe maandiko yanakiri hivyo. (Marko 13:32) Walakini habari za siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala mwana, ila Baba.

Mungu tangu aiumbe hii dunia aliiwekea utaratibu ambao inapaswa ufuatwe jua linatambua kuchwa kwake, bahari inatambua mipaka yake. (Mhubiri 3:1) Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Dunia tunayoishi sasa tupo kipindi cha neema ya wokovu, kuongoka, kukombolewa, kumwamini Yesu, kumkiri Yesu, kuokoka, kuzaliwa mara ya pili yote hayo ni jambo hilo hilo moja. Kuna muda hii neema itapigwa stop, itafunikwa, itafungwa. Mungu ni mpole sana na tena ni mkali sana, bado anatuita kwa sauti ya upole anataka ridhaa yetu twende kwake pamoja na kwamba anatulinda, anatupa pumzi,tena sehemu nyingine anatuelekeza tuchague kitu gani kati ya uzima na mauti (Kumbu kumbu la torati 30:19) Nazishuhudia mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako. (Ufunuo 3:20) Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Sharti la kwanza ni kusikia sauti yake, la pili ni kuufungua mlango (moyo) watu wengi wanasikia sauti ya Yesu ila kufungua mlango hawataki, na Mungu halazimishi mtu amfuate ingawa uwezo  anao wa kulazimisha mtu afuate vile anavyotaka. Mifano ipo mingi kutoka katika Biblia Takatifu, pia anaonyesha faida ya kumfuta na hasara ya kutomfuata. Pia ujue ya kuwa kama utakufa kabla ya tukio la unyakuo, itakuwa kwako au kwangu neema imekomea hapo baada ya kifo. Na kitakachokuwa kikisubiriwa ni hukumu tu kama ulifanya mabaya au mema yote yatakuwa na malipo yake Mungu yeye ni wa haki.

Wakati mwingine unaweza kufanya jambo la kikatiri sana ukijua ya kuwa hakuna anayekuona, ila ujue ya kuwa Mungu anaona kila pahali. (Zaburi 139:7) Niende wapi nijiepushe na roho yako? niende wapi niukimbie uso wako? na (Waebrania 4: 13) Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.
Iwapo sisi binadamu tuna uwezo wa kutengeneza vifaa vyetu kwa ufahamu wetu vyenye uwezo wa kurekodi matukio mbali mbali na kuhifadhi na kutumika pale itakapohitajika je Mungu hatakuwa zaidi yetu sisi? si lazima atakuwa ametuzidi katika teknolojia? (1Korintho 1:25) Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu. Kwa hiyo kama unafanya maovu mfano wizi, uzinzi, kutoheshimu Mungu na wazazi, kutesa wasichana wa kazi, uuaji,ubakaji na mengine yanayofanana na hayo, Acha mara moja !!! vinginevyo utakuja juta na kusema kheli ningelijua, wakati huo utakuwa umekwisha chelewa. Mungu ana njia nyingi za kuongea na watu wake, hata ujumbe kama huu kwako inaweza kuwa ni sauti ya Mungu ikitaka ujirekebishe na kuishi jinsi anavyopenda yeye, mkibilie Yesu sasa hivi usisubiri mpaka upate tatizo, twende kwa Yesu tukiwa na nguvu zetu, usisubiri mpaka uchakazwe na Shetani, na ujue ya kuwa Shetani anakutafuta uingie kwenye 18 zake akumalize ni ulinzi wa Mungu kwako unaomzuia asifanye vitu vyake. Kumbuka ni matukio mangapi yamekukosa kosa magonjwa, ajali, wachawi, njaa, misiba au unafikiri ni akiri na ujanja iliyokuwezesha kuvuka, mi nadhani hapana, ni Mungu tu aliyetuvusha salama.

Ulimwengu unaelekea mwisho, naye shetani na watumishi wake ameongeza spidi yake ya maasi akitaka kuwavuna wengi zaidi wa kwenda nao kuzimu starehe na mambo ya kisasa zaidi kila siku yanagunduliwa ili ikiwezekana huyu binadamu ajisahau katika Mungu na kung'ang'ania vya ulimwengu ambavyo ni vya muda na vinapita na dunia yake na watu wengi wataikosa mbingu sababu ya vitu vya ulimwengu, siku hizi mawakala wa Shetani wana ujasiri wa kutoa namba za simu kwa wanaotaka kujiunga na vyama vya kishetani. Tena kuna wachungaji wanaonekana na kwenye vipindi kwenye Tv wakinadi na wanatetea mawakala hao na kusema Freemason ni vyama vya watu matajiri, ni kama CCM, CUF, Chadema hawana matatizo yoyote. Na wachungaji hao hao anajinadi kuwa yeye ni tajiri kiasi ana magari sita ya kifahari tena ya kutembelea tu, Unajiuliza hivi kanisani kwao hakuna wajane, yatima na masikini wangapi ambao amewasaidia? au kuna hospitali ngapi alizotoa msaada ili kununua japo panadol tu, kusaidia huduma za kijamii? Lakini ndugu yangu jiulize kitu hiki( Mathayo 16:26) Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? jiulize binafsi na kujipa jibu mwenyewe hawa watumishi wanamtumikia mungu gani? maana hata shetani naye ni mungu wa dunia hii.
Yesu alikuja kwa ajili ya watu wote waishio duniani. (Yohana 3:16) Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye, asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Ni Yesu pekee aliyepewa jukumu la ukombozi wa roho za watu hakuna mwingine chini ya jua usidanganyike hizi ni zama za udanganyifu,  Si Askofu, Si Mtume, Si nabii, si Maria mt, Si papa Benedict, Si Muhamed, Si Omari, Si Jua, Si Jabali. (Matendo ya mitume 4:12)
Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. Ukitumainia wokovu wa roho yako kwa mwingine ndugu yangu nakujulisha kuwa fikilia mara mbili, tatu na umkimbilie mmoja tu aitwaye Yesu.

Yesu alitokea mbinguni akaja duniani, akatoka duniani tena akaenda mbinguni ni nani mwingine aijuaye njia ya kwenda kwa Mungu? huko mbinguni? (Yohana 14:3-4) Basi mimi nikienda kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia.

Dunia hii Shetani anatawala na ndie mungu wa dunia hii, kumshinda lazima uwe na mbabe kuliko yeye si ubaunsa, Shetani hapigwi kwa fimbo au jiwe, ukiwa na Yesu pekee utamshinda Shetani yeye ndie awatiaye nguvu wanaomwamini. (Wafilipi 4:13) Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. (Ufunuo 12:11) Nao wakamshinda kwa damu ya mwana kondoo, na kwa neno la uhuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao mpaka kufa.
Tenzi za rohoni no.120 beti la ...... inasema lango lile likifungwa  mara moja halitafunguliwa, yeye ni Mungu sisi ni binadamu, yeye ni muumbaji sisi ni udongo tu na udongoni tutarudi kama alivyosema haijalishi uwezo ulionao, Mungu ni wa msimamo zaidi ya mzungu, hapelekeshwi hatuna namna ya kumgeuza afanye tutakavyo sisi, hufanya vile aonavyo kuwa vema. (Yeremia  18:3-6)

Neema hii itakapofunikwa hata usali sala ya toba mara mia na zaidi Mungu hatasikia ng'o, je utamlaumu nani ? mchungaji, shehe, baba au mama? wa kujilaumu itakuwa ni wewe mwenyewe na nafsi yako, huku ukilia pasipo mtu wa kukufariji. Watumishi wa Mungu unao waamini hutawaona wakati huo, watakuwa wamesimama mbele za Mungu wakitoa hesabu ya matendo yao.

Ukimkubari Yesu kama Bwana na mwokozi wako utapokea na muhuri wa Roho Mtakatifu ambaye atakuja kwako na kuwa pamoja nawe sasa na hata milele, bila huyu Yesu huwezi kuushinda ulimwengu pamoja na mambo yake, maana Shetani ana nguvu ya kutushinda iwapo tutakuwa hatuna huyu Yesu. Roho Mtakatifu atakapokuja kwako atakusaidia jinsi ya kuenenda katika dunia hii iliyojaa kila aina ya hila za shetani (Matendo 13:10) Lakini Sauli ambaye ndiye paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho.Akasema, ewe mwenye kujaa hila na uovu wote; mwana wa ibilisi, adui wa haki yote,huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?  dunia yenye changamoto nyingi za wokovu watumishi wenye hila za kishetani, pamoja na kuwa wanalitaja jina la yesu na wanaombea watu wakapona na watumishi hao hao wanasema siku hizi kuna manabii wa uongo. Kama utakuwa umependa kujiunga na maelfu watoto, vijana kwa wazee walio katika njia ile, tafuta mahali penye utulivu na usali sala ifuatayo kwa dhati na kwa kumaanisha.

Sala:

" Bwana Yesu Kristo, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi. Sasa nageuka na kutubu na kuziacha dhambi zote nikimaanisha ... (zitaje mbele za Mungu) niwezeshe kutozirudia kabisa nijaze na Roho Mtakatifu wako aliye mwalimu na msaidizi wa kila mwamini. Pia nifute jina langu katika kitabu cha hukumu, uniandike katika kitabu cha uzima wa milele. Asante Bwana Yesu Kristo kwa kuniokoa" Amen.
SALA

Kama ulikuwa ukisali sala hiyo hapo juu kwa kumaanisha utakuwa umekwisha okolewa, umeongoka, umezaliwa mara ya pili. Kwa kuwa sasa umemwamini Bwana Yesu Kristo, vifuatavyo ni msaada kwako ili upate kusonga mbele na kuukulia wokovu.

 1.    Soma neno la Mungu Biblia Takatifu kila siku (Warumi 10: 17) na (Wakolosai 3: 16).

2.    Sali asubuhi, mchana na jioni na kila ujisikiapo kufanya hivyo. (1 Wathesalonike                 5:17)
3.    Kama sehemu unayomwabudu Mungu hawaamini Biblia Takatifu tafuta kanisa                   linalokili
         wokovu na kutoa mafundisho ya kiroho ili upate kuukulia wokovu (1Petro 2:1-2)
         (Waebrania 10:25).

4.     Usikubali kuusikiliza uongo wa Shetani (Ufunuo 3:11), (Mwanzo 3:1-19) na                         (1Petro 5:8).
 5.     Sambaza ujumbe huu kadri uwezavyo na Mungu atakuongezea kitu,                     huwezi kujua nani
         anahitaji ujumbe kama huu siku hii ya leo (Ufunuo 22: 18), (Kolosai 4:16).


               Mtumishi T.M. Omari,
               injiliyajioni@gmail.com,
              Soft & Hard Copy Gospel Tract Ministry,
              Dar es salaam.
             
   


Comments

Popular posts from this blog

KUSAMEHE NA KUSAHAU

MAASI YA DUNIANI SASA !!! SODOMA & GOMORA CHA MTOTO

MUNGU HAJAZAA WALA HAJAZALIWA !!!